Exodus 14:10-30

10 aFarao alipokaribia, Waisraeli wakainua macho yao, wakawaona Wamisri wakija nyuma yao. Wakashikwa na hofu, wakamlilia Bwana. 11 bWakamwambia Mose, “Je, ni kwamba hayakuwako makaburi huko Misri hata umetuleta tufe huku jangwani? Umetufanyia nini kututoa Misri? 12 cHatukukuambia tulipokuwa huko Misri, tuache tuwatumikie Wamisri? Ingekuwa vyema zaidi kwetu kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani!”

13 dMose akawajibu Waisraeli, “Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovu Bwana atakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena. 14 eBwana atawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu.”

15 fNdipo Bwana akamwambia Mose, “Kwa nini wewe unanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele. 16 gInua fimbo yako na unyooshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, hivyo kwamba Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini. 17 hNitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake. 18 iNao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimi Bwana nitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.”

19 jNdipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma, 20 kikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha.

21 lNdipo Mose akanyoosha mkono wake juu ya bahari, naye Bwana akayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika, 22 mnao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.

23Wamisri wakawafuatia ndani ya bahari, pamoja na farasi wote wa Farao, magari ya vita na wapanda farasi. 24 nKaribia mapambazuko, Bwana akaliangalia jeshi la Wamisri kutoka ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha. 25 oMungu akayaondoa magurudumu ya magari yao, kwa hivyo wakayaendesha kwa shida. Nao Wamisri wakasema, “Tuachane na Waisraeli! Bwana anawapigania dhidi ya Misri.”

Wafuatiaji Wazama

26Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako juu ya bahari ili maji yarudiane yawafunike Wamisri, magari yao ya vita na wapanda farasi wao.” 27 pMose akanyoosha mkono wake juu ya bahari, wakati wa mapambazuko bahari ikarudiana na kuwa kama kawaida. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji, lakini Bwana akawasukumia ndani ya bahari. 28 qMaji yakarudiana na kuyafunika magari ya vita na wapanda farasi pamoja na jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuata Waisraeli ndani ya bahari. Hakuna hata mmoja wao aliyenusurika.

29 rLakini Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, ukiwepo ukuta wa maji upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto. 30 sSiku ile Bwana akawaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wamisri, nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni mwa bahari wakiwa wamekufa.
Copyright information for SwhNEN